Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Alireza Arafi, katika hotuba ya sala ya Ijumaa ya tarehe 22 Farvardin 1403 (sawa na Aprili 11, 2025) iliyofanyika katika Muswalla wa Quds mjini Qom, alisema: tunapitia siku ngumu. Sala za Ijumaa zimekuwa ngome thabiti za mapinduzi, fahari na utukufu wa Iran, ambazo daima zimekuwa mstari wa mbele katika kutetea thamani za kiungu, malengo ya Mapinduzi ya kiislamu, na taifa la Iran.
Aliongeza: tunapaswa kuwa makini na tusisahau kwamba madhalimu wa dunia kwa karne nyingi wamekuwa na njama dhidi ya Iran, ulimwengu wa Kiislamu, na Mashariki kwa ujumla. Madhalimu hao walikuwa na njama mbili: walisema kwamba ni lazima mnyenyekee, muwe kama ng’ombe wa kutoa maziwa, na kufuata mwelekeo na ustaarabu wa Kimagharibi, au mbaki kuwa ardhi isiyo na kitu na nchi ilizofilisika.
Khatibu wa Ijumaa wa Qom akielezea kwamba mabeberu wanapendelea mojawapo ya njia hizi mbili na hasa kwa ulimwengu wa kiislamu, alisema: Mapinduzi ya Kiislamu yalikuja baada ya karne nyingi na kwa juhudi za taifa la Iran, yamebadilisha mwelekeo wa fikra za Kimagharibi na kuyaleta mataifa ya dunia kwenye njia mpya isiyojaa udhalilishwaji na unyonge.
Aliongeza kuwa: mantiki ya Mapinduzi ya Kiislamu imeleta njia ya tatu inayoelekeza kuwa: kuwa jasiri, mwenye heshima, hekima na mvumilivu. Taifa la Iran limepita njia hii. Leo, wote wamekusanyika kutaka kuiweka pembeni harakati ya kiislamu na mantiki ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo imeleta njia mpya na ujumbe mpya dunianj na kuweka mbele heshima ya kustahimili.
Taifa la Iran halitarufi nyuma
Mudiri wa Hawza alisema: leo, watu kwa kuiga mashujaa wa kishahidi, Imam mtukufu, na kwa kufuata uongozi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, wamejitokeza kusema: hatutakuwa ng’ombe wa kutoa maziwa wala hatutakubali kuwa ardhi dhalili, bali kwa hekima, ujasiri na ushujaa tutaitetea heshima ya Iran na ulimwengu wa Kiislamu, na mtaona kuwa mantiki ya Mapinduzi ya Kiislamu haitarudi nyuma kutoka njia hii yenye nuru.
Alisisitiza: kamwe hamtaona siku ambayo taifa lililosimama kwa nusu karne kwa ajili ya malengo yake litarudi nyuma. Historia ya karne zilizopita iko mbele yetu ambapo kila mara, kwa sababu ya udhaifu wa watawala, sehemu ya ardhi yetu ilichukuliwa na heshima na hadhi yetu iliibwa.
Mjumbe wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi aliongeza: uzoefu wenye nuru kwenye vita vya kujihami na zaidi ya mashahidi laki mbili, uko mbele yetu ambapo taifa la kishujaa halikuruhusu hata shubiri ya ardhi ya Iran ichukuliwe wala pembe ya heshima ya Kiislamu kuharibiwa.
Kizazi kipya kijifunze kutoka kwa waliotangulia
Aliendelea kusema: kizazi kipya, fahamuni kwamba waliowatangulia, mashujaa na mashahidi wenu walisimama na kuvumilia magumu na kuhifadhi heshima ya Iran, Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu. Hili ni somo la leo pia. Ikiwa tunataka kusimama dhidi ya maadui, tunapaswa kuzingatia masuala haya.
Mudiri wa seminari za kidini (Hawza) alisema: hili ni dai la taifa la Iran kwa ajili ya heshima na hadhi, kwamba kila hatua ichukuliwe kwa msimamo wa ujasiri na kusimama imara dhidi ya madhalimu, na kuepuka kila aina ya udhaifu na kutegemea wengine.
Lazima utayari wa kijeshi udumishwe
Imamu wa Ijumaa wa Qom alikumbushia kwamba: ni lazima tuendelee kuwa tayari kijeshi. Uvivu hauruhusiwi; usingizi wa kusahau ni hatari kubwa kwa heshima ya baadaye. Juhudi za maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia katika nyanja za nyuklia na zisizo za nyuklia, pamoja na kutatua matatizo ya watu, zinapaswa kuoewa kipaumbele na viongozi.
Aliongeza: nchi haipaswi kushinikizwa au kugawanyika kwa misingi ya mazungumzo au kutegemea nje. Watu wote na taasisi wanapaswa kufanya juhudi. Harakati yoyote ifanywe kwa mujibu wa muongozo wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi; hapaswi kuwa na jambo lolote lililolazimishwa, lililopunguzwa au kuongezwa.
Mjumbe wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi alisisitiza: tuzingatie vita vya kiakili vinavyoletwa na adui. Wametokea kila upande kujaribu kukiondolea kizazi kipya mtazamo wa juu wa imani, kujiamini na matumaini ya baadaye. Kizazi kipya kinapaswa kuwa mstari wa mbele katika harakati kubwa.
Khatibu wa Ijumaa wa Qom alisema: Muqawama umepata pigo na madhara, lakini wapinzani wasidhani kuwa harakati hiyo imekatika na wasijidanganye kuwa volkano ya Muqawama imezimika. Volkano ya Muqawama iko hai ndani ya nyoyo za waumini na haitazimika.
Alisema: mataifa ya kiislamu yamejiletea fedheha kubwa, watawala waoga, watiifu na waliopotea wamejiletea aibu kubwa. Zaidi ya watu 50,000 wameuawa kinyama. Ole wenu nyie mlio kuwa kimya. Ummah ulio na karibu watu bilioni mbili na rasilimali nyingi za kibinadamu unashuhudia watoto wa Palestina na Gaza wakiuwawa. Lakini fahamuni kuwa ndani ya nyoyo za waumini kuna msisimko wa jihadi, imani katika kustahimili, na volkano ya ghadhabu ya kiislamu ambayo itamaliza dhulma yote.
Mudirj wa Hawza alisema: taifa la Iran litaendelea katika njia ya Imam na mashahidi, njia ya kuijenga nchi, maendeleo na uwekezaji, na kupaa kileleni mwa elimu, huku wakati huo huo likilinda maadili ya Kiungu, heshima na uvaaji wa heshima, na litabaki kwenye uwanja wa kutetea wanyonge duniani huku likipaza sauti: "Hakika tupo katika ahadi!"
Makazi ni suala muhimu
Imamu wa Ijumaa wa Qom katika sehemu nyingine ya hotuba yake alisema: makazi ni suala muhimu ambalo taasisi zote zinapaswa kulizingatia ili kasi ya ujenzi wa nyumba kwa vijana iongezeke. Mpango wa makazi uangaliwe kama sehemu ya mpango wa kukuza kizazi na kuhimiza mtoto wa tatu na kuendelea. Ikiwa mzigo wa makazi utaondolewa kwa watu, nusu ya maisha yao itatulia na utulivu utapatikana katika familia.
Alisema: katika msingi wa ujenzi wa makazi, mkoa wa Qom ni miongoni mwa mikoa bora. Tunatumai kuwa kwa mtazamo sahihi wa usanifu wa jadi, wa kisunnah na kiislamu, kizazi kipya kitafaidika na juhudi hizi na viongozi walipe kipaumbele.
Ibada ni msingi wa utamaduni wa kiislamu
Ayatollah Arafi katika khutba ya kwanza alisema: mfumo wa ibada katika Uislamu unatofautiana na dini nyingine, na mfumo wa ibada katika madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s) una tofauti na madhehebu mengine licha ya kuwa na mambo ya pamoja.
Alisema: ibada ni msingi wa utamaduni wa kiislamu. Ibada huathiri nyanja zote za maisha ya mwislamu. Roho na utamaduni wa mtu binafsi na kijamii hujieleza katika unyenyekevu, kusifu na kumuabudu Mwenyezi Mungu.
Aliongeza kuwa: Mwislamu anapaswa kujitahidi kujijengea utumwa wa kweli kwa Mwenyezi Mungu, na kuifanya ibada kuwa jambo la msingi katika maisha ya kila siku, na vilevile kueneza mantiki, fikra na utamaduni wa ibada ya Mwenyezi Mungu katika familia na jamii.
Alisisitiza kuwa: mantiki ya Uislamu inasisitiza kwamba tuweke ibada kama msingi katika kujijenga binafsi, na tuhakikishe kuwa mienendo na nia zetu zinazingatia ibada kwa Mwenyezi Mungu. Vilevile, tunapaswa kuhakikisha kuwa ibada ya Mwenyezi Mungu inakuwa ni mantiki na fikra ya kijamii.
Mudiri huyu wa Hawza alisema: juhudi za kueneza fikra ya Mwenyezi Mungu ndani ya familia, kwa watoto na kizazi kipya, ni jukumu la kwanza kwa ajili ya kuilea jamii. Uislamu haumwangalii mwanadamu kama kisiwa kilichotengwa na familia au jamii.
Alisema kuwa: nyumba ni sehemu ya kwanza na eneo la msingi katika jamii, ambapo malezi ya kiitikadi, kiibada, maadili na kidini yanapaswa kufanyika. Qur’ani inasisitiza kuwa jukumu la wazazi kwa watoto si tu la kimwili, kielimu na kiuchumi, bali pia linahusisha malezi ya kimwenendo, kimadili na kiimani.
Mjumbe wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi aliendelea kusema: Baba na mama ni viongozi wa malezi ya kina, na wanapaswa kuwa na juhudi katika nyanja zote za maisha ya watoto. Watoto ni amana ya Mwenyezi Mungu, wenye vipengele vingi, na sisi tuna jukumu mbele ya kila kipengele chao.
Aliongeza kuwa: malezi ya kiibada na kumuelekeza mwanadamu kwa asili ya kuwepo ni roho ya malezi ya kiislamu. Katika Qur’ani, hadithi nyingi za manabii wa zamani kama vile Ibrahimu, Nuhu, Ismail, Yaqub, Luqman, na wengineo zimeeleza huku zikisisitiza suala hili.
Imamu wa Ijumaa wa Qom, akirejelea aya ya Qur’ani isemayo: "Mola wangu! Nifanye niwe mwenye kusimamisha Swala, na katika kizazi changu pia," alieleza kuwa: katika aya hii, licha ya kwamba Nabii Ibrahimu hakuwa na mtoto bado, lakini alikuwa na mtazamo kwa kizazi chake, na alimuomba Mwenyezi Mungu awafanye wawe wenye kusimamisha swala.
Aliendelea kusema: Nabii Ibrahimu katika sehemu nyingine anakiombea kizazi chake cha baadaye akisema: "Ewe Mola Mlezi wetu! Tujaalie tuwe ni wenye kusilimu kwako, na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe umma ulio silimu kwako." Nabii Ibrahimu alikuwa na mtazamo kwa kizazi chake na jamii za baadaye, akiomba wawe wa kusimamisha swala na miongoni mwao wainuke viongozi wa kuwaongoza kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu.
Mudiri wa seminari za kidini (Hawza) alisema: jukumu la baba na mama kwa watoto na kizazi kijacho ni malezi kamili, yanayoanzia kwenye riziki ya kimwili na kuendelea hadi ulezi wa kiroho na kiimani.
Akinukuu aya isemayo: "Enyi mlioamini! Ziokoeni nafsi zenu na jamaa zenu na Moto wa Jahannamu," alisema: hii ni miongoni mwa aya mashuhuri ya malezi. Aya hii inasema kuwa kama mnavyojilinda nyinyi wenyewe dhidi ya moto, vivyo hivyo muwalinde jamaa zenu pia.
Maoni yako